Kukamilika kwa Ujenzi wa Barabara ya Mabasi ya Mwendokasi Awamu ya Pili (BRT), utasaidia kuchochea Uchumi na kuondoa adha ya Usafiri kwa wakazi wa Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani ambao walikuwa wakitumia muda mrefu kuingia katikati ya mji kwenye Shughuli zao za kila siku.
Lee Min, ambaye ni Meneja biashara wa Kampuni ya Ujenzi ya sinohydro Corporation limited alisema kuwa mpaka hivi sasa Ujenzi huo umefikia zaidi ya asilimia 98.5, ya kukamilika kwake na kilichobakia ni umaliziaji wa vituo vya kupakia na kushushia abiria.
Aidha, Lee Min alisema kuwa ujenzi huo ambao umekuwa ukisubiliwa kwa hamu kubwa na wakazi wa mikoa hiyo miwili, unatarajiwa kukabidhiwa rasmi serikalini octoba mwaka huu, ambapo inadaiwa kuwa ujenzi huo umezingatia ujuzi na utaalamu mkubwa kulingana na matakwa ya sekta ya ujenzi wa barabara za mwendokasi.
“Ujenzi huo ni wa awamu ya pili ambao unahusisha ujenzi wa kilometa 20.3 wa miundombimu ya barabara ya mwendokasi na magari ya kawaida itakayopita barabara ya Kilwa na upande wa barabara ya Kawawa Ujenzi wake kuwa na ubora unaotakiwa”, alisema Lee Min.
Hata hivyo, Lee Min alisema kuwa utekelezaji wa mradi huo wamepitia katika kipindi kigumu kutokana na kupitia changamoto mbalimbali zikiwemo za baadhi ya madereva kutokufuata Sheria za barabarani.
“Hali hiyo ya madereva kutozingatia sheria za usalama barabarani pamoja na kupitisha magari kwenye barabara ya mwendokasi kunachangia kwa kiasi kikubwa kuharibu miundombinu ya barabara inayojengwa na kujikuta wakirudia ujenzi mara kwa mara”, Lee Min alisema.
Meneja biashara huyo, alieleza kwa masikitiko kuwa vitendo vya kujirudia rudia kwa baadhi ya madereva kutokufuta sheria za usalama barabarani hasa katika eneo la mission njia panda ya kuelekea Kijichi kunachangia sana kusababisha ajali na kufanya uharibifu wa miundombimu ya barabara.
Akizungumzia kutokea kwa kauli za upotoshaji kwenye mitandao ya kijamii Meneja Biashara huyo, alisema kuwa taarifa hizo ni za upotoshaji kwani tangu ujenzi huo uanze mwaka 2018, mradi huo umetembelewa na viongozi mbalimbali wa serikali ambao walitoa ushauri na kila hatua wanayofikia lazima mshauri wa mkandarasi na wakaguzi kutoka Wakala wa barabara nchini (Tanroad) wajilizishe kwanza ndipo waendelee na Ujenzi mwingine.
“Hizo taarifa ni siasa na sisi sio waumini wa siasa hapa ni kuhakikisha kuwa kazi zinafanyika kwa ubora mkubwa ambapo mpaka hivi sasa wapo katika hatua nzuri ya mwisho ya kukamilisha mradi huo kwa kufunga taa na tayari wahusika tanesco wako kwenye hatua za mwisho za kuwasha taa na kuna baadhi ya sehemu tayari taa zimeanza kuwaka”, alisema Lee Min.
Kwa upande wake Mhandisi Mkazi wa Kampuni ya Botex wanahusiaka na ujenzi wa vituo hivyo Mhandisi Christian Kuyonza akizungumzia kuhusina na ujenzi wa vituo hivyo, alisema kuwa madai hayo kwa sasa hayana maana yoyote kwani bado mradi haujakabidhiwa serikalini na ujenzi wa vituo unaendelea pamoja na wakaguzi wakikagua kila hatua wanayopitia na kuainisha mapungufu yaliyopo kwenye vituo hivyo na kufanyiwa kazi.
Kuyonza alisema kuwa matirio yaliyotumika katika ujenzi wa vituo hivyo vimepitishwa na wakaguzi kutoka DART, na vina ubora unaotakiwa kitaalamu kutokana na hitaji ya mwajiri.
Alisema kuwa kwenye awamu ya pili ya ujenzi vituo vya mwendokasi vitakuwa tofauti na vya awamu ya kwanza kwani awamu ya pili kati ya vituo 4 katika vituo 26 vilivyopo kwenye mradi huo ambavyo vitakuwa na huduma ya viti kwa walemavu, vipofu, wajawazito na wazee.
“Ujenzi wa vituo hivyo unatokana na ukubwa wa eneo la barabara kwani vipo baadhi ya vituo upana wake ni mdogo kutokana na mahitaji ya sehemu husika na vingine kama pale Ilala Boma karibu na ofisi ya Mkuu wa Mkua wa Dar es Salaam kinakuwa kirefu na kipana”, alisema Mhandisi Kuyonza.