Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma akiongozana na Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole Agosti 2, 2023 wametembelea Bustani iliyotengwa na Serikali ya Cuba kwa ajili ya mashujaa wa Afrika katika mji wa Havana nchini Cuba (African Heros Park).
Mhe. Mwinjuma ametembelea eneo hilo kukagua sehemu ambayo itawekwa Sanamu ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambapo mpaka sasa nchi mbalimbali zimekwishaweka sanamu za mashujaa na viongozi wao kama vile Kenya, Afrika Kusini, Misri, Namibia na DRC.
Hata hivyo, Tanzania bado haijaweka sanamu ya Mwalimu Julius Nyerere katika Bustani hiyo ambapo Ubalozi wa Tanzania nchini Cuba kwa kushirikiana na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo zimeendelea na mchakato huo ambapo upo katika hatua za mwisho kukamilika na Mhe.Mwinjuma ameahidi kusimamia mchakato huo uweze kukamilika kwa haraka.
Kila mwaka nchi husika inapoadhimisha siku ya uhuru Mabalozi hualikwa kuweka mashada aidha, wakati wa siku ya Afika mabalozi wa Afrika hukutana hapo kusherehekea.