Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania bara Mheshimiwa Anamringi Macha ameonyesha kukerwa na mabango ya kutambulisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo vijijini kuandikwa kiingereza.
Amewataka watumishi wa Sekta za Umma nchini kuhudumia Wananchi kwa kutumia lugha ya kiswahili zaidi ilikukienzi na kuongeza uelewa wa serikali inachofanya kwenye jamii.
Amesema hayo wakati akifunga mafunzo ya 19 ya Uongozi kwa Viongozi wa Taasisi na Mashirika ya Umma yaliyofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julias Nyerere huko Kibaha mkoani Pwani kwa wiki moja.
Amesema kwasasa kuna miradi mingi sana ya maendeleo inayoendelea kujengwa nchini ikiwemo ya Barabara, ujenzi wa vituo vya afya, miradi ya maji, shule na kadhalika lakini utakuta mabando mengi yanayotambulisha miradi hiyo kwa jamii yanayowekwa na Wakandarasi wazawa yameandikwa kwa kiingereza.
“Miradi hii inayomuhusu mwananchi huko vijijini unakuta hawaielewi kwasababu tu ya lugha bango lililowekwa pale hata mwananchi hajui maana ya kilichoandikwa”
“Wakati tunapowashawishi Wananchi kulipa Kodi tunatumia lugha ya kiswahili ili watuelewe lakini wakati tunapowaletea taarifa za namna fedha hizo zinachofanya katika kutekeleza kwa Wananchi tunatumia lugha ya kiingereza”
“Mkurugenzi unapokuwa na Baraza la Madiwani jitahidini taarifa zenu mnazowasilisha kwenye vikao vyenu zisomeke kwa lugha ya kiswahili hususani zile za fedha yaani unakuta kablasha kubwa kabisa linawekwa kwa lugha ya kingereza na zile taarifa za kisheria, masuala ya nayohusu ardhi unakuta zimeandikwa kwa kiingereza”
“Ili nyie Watendaji na Madiwani muweze kusomana na mueleweke vizuri kuhusu kazi mnazofanya kwaajili ya ustawi wa Wananchi na Wananchi kwa upande wao wapate uelewa kwa ufasaha kazi zinazotekelezwa na serikali yao kwa uzalendo na uadilifu wetu katika kuwatumia”
Amesema Watumishi hao watumie lugha ya kiswahili kufikisha ujumbe kwa jamii badala ya kutumia lugha za kigeni ambazo huficha maana ya kilichofanywa na serikali kwenye jamii yao.
“Nia ni mwananchi aelewe serikali yake inafanyakazi gani sio mnaficha ujumbe katika lugha za kigeni kama kingereza lugha ambazo humnyima uelewa mwananchi” amesema Mheshimiwa Macha.
Akitoa mfano wa makosa yanayofanywa na Watumishi wa Umma kwenye baadhi ya mambo kuwa ni pamoja na kuweka mabango ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Sekta ya maji au ujenzi wa Barabara vijijini kwa kuwekwa maelezo kwa lugha ya kingereza na kusababisha wanavijiji kutoelewa kitu ambacho Serikali inafanya katika mradi huo.
Amesema lugha za kigeni zinahitajika nchini baadhi ya mambo kama katika Shule na vyuo ili kufundisha wanafunzi lakini sio katika kufikisha ujumbe kwa Wananchi hasa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa jamii.
“Bado tunahitaji lugha ya kingereza katika kufundisha wanafunzi Shuleni na vyuoni lakini sio katika kufikisha ujumbe kwa Wananchi wetu ni serikali yao imetekeleza kwao” amesema Macha.
Aidha amewataka Wahitimu 56 wa Mafunzo hayo kwenda kuonyesha walichofundishwa kwa vitendo “Mafunzo haya yakawasaidie kufanya mabadiliko katika taasisi zenu katika kuwahudumia Wananchi kwani ukosefu wa uzalendo, uadilifu, uaminifu na utawala Bora haina maana nyinyi kupata Mafunzo haya”
Awali akimkaribisha Mgeni rasmi Mkuu wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julias Nyerere Prof. Marcelline Chijoliga amesema mafunzo hayo yalikuwa na washiriki 56 na kwamba tangu shule hiyo ianze washiriki 2019 kutoka nchi za Africa kusini, Angola, Zimbabwe, Namibia, Msumbiji na Tanzania ambazo zimefadhiriwa na Chama Cha kikomunisiti Cha China na kwamba taasisi 40 zimekitumia chuo hicho.
Aidha Prof. Chijoliga amezitaka taasisi za Serikali na Mashirika ya Umma na Chama kutumia Shule hiyo kwa Mafunzo ya Uongozi kwa Watumishi wake ilikuleta tija kwa taifa ikiwa ni pamoja na kuenzi lengo la Baba wa Taifa Mwalimu Julias Nyerere kuanzisha shule hiyo.
Mwenyekiti wa Darasa hilo la Mafunzo ambaye pia ni Mhandisi Mwandamizi wa TCRA Kadaya Baluhuye akielezea changamoto waliyokutana nayo Shuleni hapo kuwa ni pamoja na kukosekana kwa Nishati ya umeme na huduma za mawasiliano ya simu za uhakika licha ya shule hiyo kutumiwa na wageni kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Naye Mshiriki wa Mafunzo hayo kutoka Taasisi ya Mwalimu Julias Nyerere ambaye ni Katibu wa Mkoa wa Pwani Omary Punzi ameshukuru kwa Mafunzo waliyopata ambayo yatawajengea Moyo wa uzalendo katika kuwahudumia taifa na Wananchi kwa ujumla.
Mshiriki Mwalimu wa kike mwenye watoto mapacha wa miezi 7 Anastasia Paul amewataka Wanawake wajawazito na wenye watoto wadogo wasiache kwenda kushiriki Mafunzo katika Shule hiyo kwakuwa Shuleni hapo Kuna mazingira rafiki kwa mama wenye watoto wadogo na pia wanaruhisiwa kuwa na wasaidizi kwa kulea Watoto.