Ousmane Sonko, ambaye anazuiliwa tangu Julai 31, alihamishwa Jumapili Agosti 6 hadi idara ya dharura ya hospitali huko Dakar. Kiongoi huyo wa upinzani nchini Senegal ambaye alianzisha mgomo wa kula tangu kufungwa kwake, ana hali mbaya kiafya, kulingana na chama chake cha kisiasa, PASTEF, ambacho kiliweka habari hiyo hadharani.
Ousmane Sonko alihamishwa katika hospitali kuu ya Dakar, mojawapo ya hospitali kubwa katika mji mkuu wa Senegal. Taarifa tulizopewa na afisa mkuu wa mamlaka ya gereza, ambaye anatufafanulia kuwa ni hatua iliyochukuliwa kwa ushauri wa daktari wa gereza la Sebikotane, ambapo mpinzani huyo wa Senegal anafungwa tangu Julai 31.
Ousmane Sonko amekuwa kwenye mgomo wa kula kwa siku nane na hali yake ya afya imedorora, “na kulazimu kuwekwa chini ya uangalizi wa matibabu katika hospitali kuu”, anatuambia mmoja wa viongozi wa chama cha PASTEF.
Chanzo hiki kinatufahamisha kwamba, akiwa kwenye kitanda chake cha hospitali, Ousmane Sonko aliwafahamisha mawakili wake kwamba hataki kusitisha mgomo wake wa kula, huku akiwaomba wafungwa wengine katika magereza ya Senegal “kukomesha aina hii ya upinzani”.
Yeye mwenyewe aliwatolea wito wale wanaoitwa wafungwa wa kisiasa kuanzisha mgomo wa kula. Baadhi walikuwa wamefuata agizo hili.
Baadhi ya wafungwa hao wamelazwa katika hospitali za Senegal, huku wafungwa wa kike katika gereza la wanawake pia wamekuwa kwenye mgomo wa kula kwa wiki moja.