Antonio Guterres amesema katika ujumbe wake kwamba wakati huu ambapo baadhi ya nchi zinatishia kutumia silaha za nyuklia, kivuli cha vita vya nyuklia kinaonekana tena kwenye sayari ya dunia.
Katika ujumbe huo, Antonio Guterres ametoa wito wa kutupiliwa mbali kabisa silaha za nyuklia, akisisitiza kuwa suala la kuharibu silaha za nyuklia bado ni kipaumbele cha juu cha sera ya upokonyaji silaha ya Umoja wa Mataifa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameendelea kwa kusisitiza kwamba, njia pekee ya kuondoa hatari ya nyuklia ni kuharibiwa silaha za nyuklia na kusema: Hatutatulia hadi kivuli cha nyuklia kitakapoondolewa kikamilifu.
Wanajeshi wa Marekani walifanya shambulio la kwanza la bomu la atomiki katika historia ya mwanadamu kwa kushambulia miji ya Hiroshima na Nagasaki huko Japan mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia. Mashambulizi haya na silaha za nyuklia ya Marekani dhidi ya watu wa Japan ndio mfano pekee wa matumizi ya silaha za nyuklia katika mzozo wa kijeshi katika historia ya mwanadamu.
Takwimu zinaonyesha kuwa, shambulizi la bomu la nyuklia huko Hiroshima pekee lilisababisha vifo vya kati ya watu elfu 70 na laki moja kwa siku moja tu. Mwishoni mwa 1945, idadi ya wahanga waliouawa katika hujuma hiyo ya mabomu ya nyuklia iliongezeka hadi watu laki moja na elfu 40 kutokana na wale waliofia hospitalini kwa majeraha na mionzi ya nyuklia.