Maafisa watano wa jeshi la wanamaji la Uganda waliokuwa katika harakati ya kuopoa miili ya watu waliozama katika ajali iliyotokea wiki iliyopita katika Ziwa Victoria wameokolewa hapo jana Jumapili baada ya mashua yao ya uokoaji kupinduka, polisi katika taifa hilo la Afrika Mashariki wamethibitisha.
Takriban watu 20 walifariki katika ajali hiyo Jumanne iliyopita iliyohusisha boti iliyokuwa imejazwa mizigo ikidaiwa kuwa raia 34 walikuwa wameabiri chombo hicho. Watu tisa waliokolewa huku wengine wakiwa hawajulikani waliko.
Siku ya Jumamosi, polisi walisema walikuwa wameopoa miili mitano tu, yote ikwia ni ya wanawake, maofisa nchini humo wakisema wanakabiliwa na changamoto kutokana na hali mbaya ya hewa kwenye ziwa hilo kutokana na mvua kubwa inayoendelea.
Licha ya hayo, maofisa wa polisi wanasema uchunguzi wa ajali hiyo unaendelea na taarifa zaidi itatolewa baada ya shughuli hiyo kukamilika wakati huu pia utafutaji wa miili ya watu waliozama ikiwa bado inaendelea.