Idadi kubwa ya watu wameidhinisha mabadiliko ya katiba ya Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa zaidi ya asilimia 95 ya kura, kamati inayosimamia kura ya maoni ilisema katika matokeo yake ya awali.
Vyama vya upinzani na baadhi ya mashirika ya kiraia yalisusia kura hiyo, yakisema sheria iliyofanyiwa marekebisho iliundwa ili kumweka Rais Faustin-Archange Touadéra madarakani maisha yake yote.
Walisema kura hiyo ya maoni imekosa uwazi na kuna muda mfupi uliotolewa kujadili vifungu vyake. Takribani watu milioni mbili walijiandikisha kupiga kura, na waliojitokeza walikadiriwa kuwa wachache.
Sheria inayopendekezwa inafuta ukomo wa mihula miwili ya urais na kuongeza muda wa kukaa madarakani kutoka miaka mitano hadi saba.
Pia inapiga marufuku wanasiasa wenye uraia wa nchi mbili kugombea urais.
Chini ya mapendekezo ya mabadiliko hayo, kutakuwa na ofisi ya makamu wa rais, itakayoteuliwa na rais. Bunge la seneti litafutiliwa mbali, na kubadilisha bunge kuwa moja. Idadi ya majaji wa mahakama kuu imeongezwa kutoka tisa hadi 11, na rais na bunge la taifa sasa wanaweza kuchagua majaji watatu kila mmoja.
Hapo awali waliweza kuchagua mmoja tu. Rais na wanachama wa chama chake cha United Hearts wamedai kuwa wanafuata matakwa ya wananchi.
Upinzani umeyaita “mapinduzi ya kikatiba”. Rais Touadéra amejitahidi kukomesha makundi ya waasi ambayo yamekuwa yakidhibiti maeneo makubwa ya nchi tangu aingie madarakani mwaka 2016, tukio lililotokana na uasi mwingine mwaka 2013 ambao ulimwondoa madarakani aliyekuwa Rais François Bozizé.
Aliigeukia Urusi kwa usaidizi wa kukabiliana na waasi mwaka 2018.