RAIS Samia Suluhu Hassan leo Jumanne amezindua programu ya uchimbaji wa visima kwa ajili ya wakulima wadogo 67,850 kwa nchi nzima zitakazowezesha jumla ya hekari 2,7014,000 kufikiwa na mfumo wa umwagiliaji.
Akitoa maelezo kwa Rais Samia katika maonesho ya kilele cha sherehe ya wakulima nane nane kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema kila kisima kitakuwa na uwezo wa kuhudumia wakulima 16.
Amesema kisima hicho kitakuwa na tenki la lita 5000 litakalokuwa limefungwa mfumo wa umeme jua (sola panel) kwa ajili ya ku-pump.
“Pia mkulima atapewa eneo la umwagiliaji la heka 2.5 na mkulima wa kwanza katika program hii anatoka wilayani Mbarali mkoani Mbeya,” amesema.
Aidha, akizungumzia mradi huo, Rais Samia amempongeza Bashe kwenye eneo hilo umwagiliaji maji kwa kufanikiwa kutumia vyanzo mbalimbali ikiwamo skimu za umwagiliaji.
Hata hivyo, amesema upo uwezekano wa kutumia maziwa ambayo Mungu ameibariki Tanzania yakatumika pia katika kilimo cha umwagiliaji.
“Tunalo Ziwa Vicktoria, Tanganyika na Nyasa maji yako pale. Tukivuta maji machache kufanyia kilimo haitadhuru samaki waliokuwepo pale wala haitapunguza kina cha maji cha meli kuelea, ni maziwa makubwa Mungu katubariki.
“Angalieni uwezekano wa kutoa maji kumwagilia kwenye mashamba wakulima wavune mara mbili kwa mwaka,” amesema.
Ametoa mfano kuwa nchi kama Misri inatumia maji ya Mto Nile kuzalisha ngano ambayo imeifanya nchi hiyo kuwa kinara wa uzalishaji wa zao hilo duniani.
“Kuwepo mikataba sijui ya kikanda wenzetu wamefumba macho na masikio. Sisi Mungu katupa maziwa matatu alafu tunatafuta vyanzo vya kumwagilia kilimo! vitumiwe watalaamu wakae ili kilimo chetu kikue zaidi,” amesema.