JUMLA ya vijana 420 kutoka Tanzania Bara na Visiwani wanatarajiwa kujiajiri kupitia mafunzo waliyopatiwa na Serikali kwa ajili ya kuwatengenezea wakulima vihenge vitakavyowasaidia kudhibiti sumu kuvu.
Hayo yamebainishwa leo na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe wakati akitoa maelezo kwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alizindua mradi huo na kuwapatia baadhi ya vijana hao vitendea kazi.
Rais Samia alikuwa mgeni rasmi katika kilele cha sherehe za wakulima Nane nane zilizofungwa leo tarehe 8 Agosti 2023 katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.
Akifafanua kuhusu mradi huo wa sumu kuvu, Bashe amesema serikali imeshirikiana na watalaam wa VETA, Wizara ya elimu kuwapatia mafunzo vijana hao 420 namna ya kutengeneza vihenge.
“Kwa hiyo vijana 420 kutoka nchi nzima ikiwamo Zanzibar utawakabidhi vitendea kazi wawakilishi wao ambao watafanya kazi na mkulima kuwatengenezea vihenge na kuwauzia. Itakuwa ni sehemu ya ajira kwao hasa ikizingatiwa ni vijana waliopewa mafunzo na serikali na wamepewa vifaa vya kutengenezea vihenge hivyo,” amesema.