Katika kuhakikisha Vijana wengi wa Kitanzania wanapata ujuzi utakaowazesha kuacha kukaa vijiweni na kupata ajira ili kujikomboa na umasikini, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari kupitia Chuo cha Bandari imeondoa kigezo cha Mtu kuwa na cheti cha form four au cheti kingine chochote cha taaluma ili apate mafunzo ya kuendesha mitambo mikubwa na midogo ambapo kwa sasa kigezo cha kupata kozi ni kuwa na leseni ya Udereva tu.
Awali kozi za muda mfupi za uendeshaji wa Mitambo mikubwa na midogo zilikuwa zinamlazimu Mtu kuwa na vyeti vingi ikiwemo vya elimu kuanzia form four na hivyo kuwakwamisha Watanzania wengi kukosa nafasi kwa kukosa sifa lakini kwa sasa kigezo kikubwa cha kujiunga kozi hizo ni leseni tu.
Akiongea wakati wa Maonesho ya Wakulima NaneNane Kanda ya Mashariki Mjini Morogoro Mratibu wa Mafunzo kutoka Chuo hicho John Kambona amesema wameboresha sifa za kujiunga na kozi hizo ili kutoa fursa kwa Watanzania wote ambao wanahitaji kujifunza kuendesha mashine hizo kuchangamkia fursa hiyo ili waache kukaa vijiweni wakilalamikia ukosefu wa ajira.
Kambona amesema katika kozi hizo Washiriki wa mafunzo wanasoma kwa Wiki moja tu darasani na wiki tatu watakua Bandarini wakifanya mafunzo kwa vitendo na baada ya hapo wanakuwa wameiva na kuchangamkia fursa za ajira Bandarini ili Watanzania wengi wanufaike na ajira za Bandari na maeneo mengine yanayotumia mitambo hiyo.