NAIBU Waziri wa Tamisemi Deogratius Ndejembi amemuahidi Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi mkoa wa Tanga kutembelea maeneo yote yaliyopitiwa na Mwenyekiti huyo wakati wa ziara yake.
Hayo yamebainishwa wakati wa mwendelezo wa ziara ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa Tanga Rajabu Abdurahman alipokagua Zahanati ya Magila gereza iliyopo Kijiji cha Magila kata ya Magaila Wilayani Korogwe ambayo takbriban miaka sita haijamalizika.
Ndejembi alizungumza na wananchi na wanaccm waliombatana na Mwenyekiti huyo kwenye ziara yake kwa njia ya simu kuwa kweli Mh,Rais anatoa pesa nyingi kwa ajili ya kugusa maisha ya Watanzania kwenye miradi mbalimbali ya kimaendeleo.
Katika hatua nyingine Waziri huyo pia alimuomba Mbunge wa Korogwe Vijijini akutane nae Bungeni mjini Dodoma ili wakae pamoja na kuona namna ya kuimalizia Zahanati hiyo ili wananchi waweze kupata huduma ya afya kwa urahisi.
“Kwanza nikupongeze Mwenyekiti kwa kufanya ziara hiyo na ndio namna ya kuisimamia ilani ya Chama chetu nikuahidi sitokuangusha nitapita kila ulipopita na nitashughulikia kero zote za ucheleweshwaji wa miradi ya kimaendeleo”Alisema Ndejendi.
Kwa upande wake Mwenyekiti huyo alimwambia Naibu waziri huyo kuwa baada ya ziara hiyo wataandika taarifa rasmi ya miradi yote iliyokwama ili Wizara hiyo iweze kutafuta majibu ya sababu zinachopelekea miradi hiyo isimalizike kwa wakati.
“Changamoto ni kubwa mbali ya kutokumizika kwa zahanati hii ya magila lakini katika vituo vya afya vya Kerenge na Mnyuzi na wasiwasi wangu pesa zake zisije kuwa zimeliwa,vina muda mrefu na havimaliziki”Alisema Rajabu.
Nae Mbunge wa Korogwe Vijijini Timotheo Mzava alisema mwaka 2017 wananchi wa Kijiji hicho cha Magila walianzisha ujenzi wa Zahanati hiyo ya Magila gereza ili waweze kujikwamua na changamoto ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma ya afya.
“Wananchi walianzisha mradi huu wa Zahanati na nilijitahidi kuwaunga mkono lakini bado kunahitajika nguvu ya Serikali kumalizia Zahanati hii”Alisema Mzava.
Mganga mkuu wa Wilaya Korogwe Miriam Cheche alisema kweli wananchi hao walianzisha ujenzi wa zahanati hiyo ingawa bado haijaingia kwenye mfumo wa Serikali wa kutengewa fungu la kuimalizia.