Miamba hao wa Ujerumani wamekuwa wakijaribu kumsajili Kane kwa wiki kadhaa na hatimaye wamefikia makubaliano baada ya Tottenham kukubali dau linaloaminika kuwa la zaidi ya pauni milioni 86.4 siku ya Jumatano.
Kane lazima sasa aamue kama atahamia Allianz Arena au la.
Kane alitaka kusuluhisha hali hiyo kabla ya safari ya Tottenham kwenda Brentford wikendi hii, na baada ya ofa kufeli na duru kadhaa za mazungumzo, Bayern wamekubali pendekezo na Spurs.
Lakini mchezaji huyo wa kimataifa wa Uingereza anafikiriwa kufurahia maisha chini ya bosi mpya Ange Postecoglou na amekuwa akiegemea kusalia.
Lakini habari za makubaliano ya Bayern na Tottenham huenda zikamshawishi Kane kuihama klabu hiyo.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30 kwa sasa amebakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake na Spurs na bado hajaonyesha dalili za kujituma kwa muda mrefu, ingawa Daniel Levy ana nia ya kumfunga mfungaji bora wa muda wote.