Nchini Niger, Jenerali Abdourahmane Tchiani, ametangaza baraza la serikali ya mpito licha ya wito wa kumrejesha madarakani rais Mohamed Bazoum.
Serikali mpya inaundwa na mawaziri 21, wakiwemo mawaziri wawili wa serikali na mjumbe wa waziri.
Serikali mpya ya mpito, inayoundwa na watu wa kijeshi na raia, inaongozwa na waziri mkuu wa muda Lamine Zeine Ali Mahamane, ambaye pia ataongoza wizara ya uchumi na fedha.
Aliyekuwa mkuu wa wafanyikazi Luteni Jenerali Salifou Mody, anayeonekana kuwa naibu wa Jenerali Tchiani, ameteuliwa kuwa waziri wa ulinzi wa kitaifa.
Kanali Meja Abdourahmane Amadou, ambaye amekuwa akisoma taarifa nyingi kwenye Televisheni ya serikali tangu mapinduzi ya Julai 26, ni waziri wa vijana na michezo.
Tayari jeshi hilo limewataja wakuu wapya wa kijeshi na kuwafuta kazi maafisa wengi wakuu wa serikali waliohudumu katika utawala wa Bazoum.