Wakuu wa nchi za Afrika Magharibi wanakutana kujaribu kuamua iwapo watahitajika kutumia nguvu za kijeshi au diplomasia kurejesha demokrasia nchini Niger.
Maofisa wa jeshi nchini humo bado wanamshikilia rais wa Niger aliyeondolewa madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi ambayo yameonekana kuendelea kufanyika katika ukanda huo wa Afrika Magharibi. Wakuu wa Ecowas wanakutana mjini Abuja nchini Nigeria.
Viongozi hao wamekuwa wakiendelea kutafuta suluhu ya kurejesha utawala wa kidemokrasia katika taifa hilo linaloendelea kukabiliwa na utovu wa usalama kutoka kwa makundi ya watu wenye silaha.
Licha ya wito kutoka kwa jamii ya kimataifa wa kutaka kurejeshwa kwa utawala wa kiraia nchini humo, wanajeshi waliotekeleza mapinduzi hayo wameonekana kutoitikia wito huo.
Ecowas chini ya Uenyekiti wa Nigeria awali ilikuwa imetishia kutumia nguvu za kijeshi iwapo uongozi wa kiraia hautarejeshwa.
Nchi jirani ya Mali ambayo nayo pia imekuwa ikikabiliwa na mapinduzi ya kijeshi na ambayo inaungwa mkono na mamluki wa Urusi, imeunga mkono wanajeshi walioongoza mapinduzi nchini Niger.