Tunisia na Libya zilitangaza Alhamisi kuwa wamekubaliana kugawana jukumu la kutoa makazi kwa mamia ya wahamiaji waliokwama kwenye mpaka wao, wengi wao kwa zaidi ya mwezi mmoja.
Wahamiaji hao, hasa kutoka nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, walikuwa wamefukuzwa hadi eneo la jangwa la Ras Jedir na mamlaka ya Tunisia na kuondoka huko ili kujilinda wenyewe, kulingana na mashahidi, mashirika ya haki za binadamu na mashirika ya Umoja wa Mataifa.
Makundi ya misaada yalisema makundi matatu ya wahamiaji wapatao 300 kwa jumla yamesalia huko.
Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ya Tunisia, Faker Bouzghaya, alisema wakati wa mkutano wa pamoja na mamlaka ya Libya mjini Tunis kwamba “tumekubali kugawana makundi ya wahamiaji ambao wako mpakani”.
“Tunisia itasimamia kundi la wanaume 76, wanawake 42 na watoto wanane,” Bouzghaya aliiambia AFP.
Alisema makundi hayo yalihamishwa siku ya Jumatano hadi vituo vya mapokezi katika miji ya Tatouine na Medenine na kupatiwa huduma za kiafya na kisaikolojia, kwa usaidizi wa Hilali Nyekundu ya Tunisia.