Meli kubwa ya mizigo ya MV Nordic Bc Munich yenye urefu wa mita 180 na kina cha mita 7.4 kutoka nchini India imetia nanga kwa mara ya kwanza katika Bandari ya Tanga ikiwa imebeba shehena ya mabomba kwa ajili ya mradi mkubwa wa maji Mkoani Tanga wa kutoa maji kutoka Mto Pangani kwenda katika Miji ya Pangani, Muheza, Korogwe na Handeni.
Afisa Masoko na Huduma kwa Wateja wa Bandari ya Tanga, Habiba Godigodi amesema kufika kwa Meli hiyo ni matunda ya maboresho makubwa ya Ujenzi wa gati mpya yenye urefu wa mita 450 pamoja na uongezaji wa kina cha bandari ili kuruhusu Meli kutia nanga na kugeuza kwa urahisi.
Akiongea wakati wa Kilele cha Maonesho ya Nanenane Mjini Morogoro, Habiba amesema uboreshaji huo ambao umetumia Shilingi Bilioni 429, umewezesha kujengwa kwa gati yenye urefu wa mita 450 na pia kuongeza njia ya kupitishia Meli yenye urefu wa kilomita 1.7 na upana wa mita 700 na hivyo kuwezesha Meli kutia nanga katika bandari hiyo na kupakua mizigo kwa urahisi tofauti na awali ambapo mizigo ilishushwa mbali na kupakiwa katika Matishari ili kufikishwa bandarini.
Itakumbukwa mwezi February mwaka huu Meli kubwa ya mzigo kutoka nchini Urusi yenye urefu wa mita 150 ilitia nanga kwa mara ya kwanza kwenye Bandari ya Tanga kisha baadaye mwezi March mwaka huu Bandari ya Tanga ikapokea Meli nyingine kubwa kutoka China ikiwa na shehena ya mizigo na magari.