Malawi imeomba msaada ili iweze kusambaza chakula kwa zaidi ya wakimbizi 50,000 wanaokabiliwa na uhaba katika kambi pekee ya wakimbizi nchini humo, wakati maafisa wa serikali wakisema akiba ya chakula itakwisha kabisa mwezi Decemba.
Ombi hilo limetolewa baada ya shirika la Chakula Duniani ,WFP kupunguza kwa nusu resheni ya chakula kwa wakimbizi hao, kutokana na kupungua kwa ufadhili.
Wakimbizi hao kwenye kambi ya wakimbizi ya Dzaleka wanasema uhaba wa chakula umekuwa mbaya sana kwasababu ya kuendelea kwa kuwahamisha wakimbizi sehemu nyingine, ambao wamekuwa wakikaa nje ya kambi.
Serikali ya Malawi ilianza kuwahamisha wakimbizi na waomba hifadhi mwezi Juni kwa mujibu wa sera ya wakimbizi, inayowataka kuishi na kufanyia shughuli zao ndani ya kambi.
Maafisa wa serikali wamesema kwamba zaidi ya wakimbizi 2,000 miongoni mwa 8,000 waliolengwa tayari wamehamishiwa kwenye kambi.
Mwezi uliopita, WFP ilipunguza mgao wa chakula kwa wakimbizi kwa nusu kutokana na matatizo ya ufadhili, wakati ikiomba msaada wa dola milioni 6.3, ili kukidhi mahitaji ya chakula kwa wakimbizi hao hadi Juni mwaka ujao.
Waziri wa Usalama wa Ndani wa Malawi Ken Zikhale Ng’oma Jumatano wakati akihutubia wanahabari amesema kwamba hatua ya kupunguzwa kwa misaada ya chakula imeiacha serikali katika hali ngumu.