Mamlaka nchini Ethiopia imesema imekuwa ikiendeleza oparesheni dhidi ya hoteli, baa na maeneo ya burudani katika mji mkuu ambapo inadaiwa vitendo vya mapenzi ya jinsia moja na ushoga vinafanyika.
Ofisi ya utawala wa amani na usalama ya Addis Ababa,ilisema ilikuwa ikichukua hatua “dhidi ya taasisi ambazo vitendo vya ushoga vinatekelezwa”.
Katika taarifa yake kwenye mtandao wa Facebook, mamlaka ya jiji hilo ilisema hatua hiyo ilikuja baada ya taarifa kutoka kwa umma, na kusema kuwa tayari ilikuwa imevamia nyumba ya wageni.
Wananchi wametakiwa kutoa taarifa kwa polisi kuhusu vitendo hivyo, serikali ikisema kuwa itaendelea na msako katika maeneo mengine.
Mapenzi ya jinsia moja ni marufuku nchini Ethiopia, lakini hakujawa na ripoti zozote za hivi majuzi za kesi au hatia zinazohusiana na vitendo vya ushoga.
Mapema wiki hii, kikundi cha utetezi kinachowakilisha wapenzi wa jinsia moja, House of Guramayle, kilisema Ethiopia ilikuwa ikishuhudia “mashambulio ambayo hayajawahi kushuhudiwa kwa watu binafsi kulingana na mwelekeo wao wa kijinsia halisi au unaofikiriwa na utambulisho wa kijinsia”.
Ilitoa wito kwa mashirika ya kutetea haki za binadamu mashinani na kwingineko kulaani mashambulio kama hayo, na kuhimiza majukwaa ya mitandao ya kijamii kushughulikia video za matamshi ya chuki zinazoitisha vurugu.