Russia imesema imefanikiwa kutungua ndege 11 zisizo na rubani za Ukraine karibu na eneo la Crimea, na nyingine mbili zilizokuwa zinaelekea Moscow.
Wizara ya Ulinzi ya Russia imesema katika taarifa ya jana Alkhamisi kuwa, mifumo ya ulinzi wa anga ya nchi hiyo imetungua droni 11 za Ukraine zilizokuwa zikiruka karibu na anga ya Crimea, na nyingine 2 nje ya mji mkuu Moscow.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa: Droni 2 za Ukraine zimetunguliwa karibu na jiji la Sevastopol, pwani ya Crimea, na nyingine tisa zimesambaratishwa kupitia vita vya kielektroniki na zikadondoka kwenye Bahari Nyeusi.
Huku hayo yakijiri, Meya wa jiji la Moscow, Sergey Sobyanin ametangaza habari ya kutibuliwa shambulizi jingine la droni dhidi ya mji huo mkuu wa Russia.
Amesema, “Alfajiri ya Alkhamisi, Vikosi vya Ulinzi wa Anga vimedungua droni mbili za kijeshi zilizokuwa njiani kuelekea Moscow. Moja ilitunguliwa katika eneo la Kaluga na nyingine karibu na barabara kuu ya Central Ring.”
Wakati huo huo, Dmitry Medvedev, Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Usalama wa Taifa la Russia, amesema kuwa nchi yake ina vikosi vya jeshi vya kutosha kutekeleza majukumu yote ya operesheni maalumu ya kijeshi nchini Ukraine.