Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Jokate Mwegelo @jokatemwegelo amesema hatokubali kukwamishwa na Mtumishi yeyote ambaye atakuwa Mzembe katika kusimamia miradi ya maendeleo na hivyo kushindwa kufikia adhima ya Rais Dkt. Samia kupeleka miradi mbalimbali ya maendeelo kwa Wananchi.
DC Jokate ameyasema hayo katika ziara ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga Rajabu Abdallah wakati akikagua mradi wa Shule mpya ya msingi ya Old Korogwe ambapo ujenzi wake hadi kukamilika utagarimu takribani Tsh.milioni 350 ikiwa ni fedha inayotokana na programu maalumu ya BOOST.
“Ndugu Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga sisi korogwe tumedhamiria kwa dhati kabisa kutimiza adhima ya Mhe. Rais katika kuwaletea Wananchi maendeleo kwani Rais analeta fedha nyingi kwenye Wilaya yetu katika Sekta mbalimbali kama Afya, Elimu, Miundombinu ya barabara na mingine mingi hivyo sisi kama Viongozi aliotupa dhamana hatutakubali kuona fedha za Mhe.Rais zinaliwa na wachache wasiotimiza wajibu wao hatutokubali”
Kwa upande wake Mwenyekiti huyo amepongeza juhudi hizo na kusema kuwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo ndio huleta chachu ya Wananchi kuweza kushiriki kwenye ujenzi kwani Wananchi wanakuwa sehemu ya miradi inayotekelezwa kwenye maeneo yao.