Rais wa Iran Ebrahim Raisi amewaagiza Waziri wa Mambo ya Ndani Ahmad Vahidi na Gavana wa Mkoa wa Fars Mohammad Hadi Imaniyeh wawatambue haraka na kuwaadhibu wahusika wa shambulio la kigaidi huko Shah Cheragh mjini Shiraz.
Katika mazungumzo tofauti ya simu, Raisi, ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza Kuu la Usalama la Taifa (SNSC), amewataka maafisa hao wawili kutumia kikamilifu uwezo uliopo kwa ajili ya kuwahudumia waliojeruhiwa.
Raisi amesisitiza kuwa wale wote ambao kwa namna fulani wamehusika katika shambulio hilo la kigaidi lazima watambuliwe na kufikishwa mahakamani.
Ametuma salamu zake za rambirambi kwa familia zilizofiwa na za waathiriwa.
Katika chapisho kwenye akaunti yake ya X ,waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian amelaani vikali shambulio hilo la kigaidi na kuonya kuhusu “mwisho wenye uchungu” kwa waliohusika na jinai hiyo.
Haram ya Shah Cheragh huko Shiraz lilikuwa eneo la shambulio kama hilo la magaidi wenye silaha mwaka jana.
Vyombo vya habari vya serikali vimeripoti magaidi wawili walihusika katika ufyatuaji risasi siku ya Jumapili.
Mmoja wa washambuliaji amekamatwa na mwingine anasemekana kuwa ametoroka.
Watatu kati ya waliojeruhiwa wako katika hali mbaya.
Kundi la kigaidi la ISIS au Daesh lilidai kuhusika na hujuma hiyo mbaya.