Mamlaka nchini India, imesema takriban watu 24 wameuawa, tisa kati yao wakifariki baada ya hekalu kuporomoka na makumi ya wengine wakiwa hawajulikani waliko kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi nchini humo.
Mvua hiyo kubwa inayoendelea nchini humo, imesababisha pia kusombwa kwa magari, kubomoa majengo na kuharibu madaraja katika majimbo ya kaskazini ya Uttarakhand na Himachal Pradesh.
Mafuriko na maporomoko ya ardhi ni ya kawaida na husababisha uharibifu mkubwa wakati wa msimu wa mvua kubwa nchini India, lakini wataalam wanasema mabadiliko ya hali ya hewa yanaongeza kasi ya kinachoendelea kwa sasa.
Sukhvinder Singh Sukhu, waziri mkuu wa jimbo lililoathiriwa zaidi Himachal Pradesh, amesema watu wasiopungua 16 wamepoteza maisha katika muda wa saa 24 zilizopita, wakiwemo tisa katika tukio la kuanguka kwa hekalu la Kihindu katika mji mkuu wa jimbo la Shimla.
Sukhu alitoa wito kwa wakazi kukaa ndani na kuepuka kwenda karibu na mito. Shule katika jimbo hilo zilikuwa zimefungwa.