Mapigano yamezuka upya kati ya jeshi la Sudan na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) katika jimbo la Darfur Kusini, magharibi mwa Sudan, wakati mapambano ya kikabila yakiendelea jimboni humo.
Kulikuwa na ripoti zenye utatanishi kuhusu idadi ya vifo na majeruhi kutokana na mapigano ya kijeshi na ghasia za kikabila. Taarifa ya kikosi cha RSF imesema, raia zaidi ya 43 wakiwemo watoto na wanawake wanane, wameuawa katika mashambulizi ya kiholela ya mizinga dhidi ya makazi kadhaa huko Nyala, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kusini.
Jeshi la Sudan bado halijajibu shutuma hizo, lakini vyombo vya habari vya huko na mashuhuda, vimesema watu wengi wamepoteza maisha katika mapambano ya kikabila jimboni humo.
Mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, Volker Perthes, alionya mwezi Julai kwamba mzozo huo haukuonyesha dalili za utatuzi wa haraka na “unahatarisha kubadilika kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyo na maadili.”
Juhudi za upatanishi wa kidiplomasia hadi sasa zimeshindwa na usitishaji mapigano umetumiwa na pande zote mbili kujipanga upya.