Kamishna wa Uhifadhi wa Wanyamapori (TAWA), Mabula Misungwi Nyanda amesema Serikali kwa kushirikiana na Taasisi zake imeweka mikakati ya kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu ikiwemo matumizi ya teknolojia katika kuwadhibiti kwa kuwaua na kuwavuna ili wasilete madhara zaidi.
Mabula amesema hayo katika kikao cha hadhara na Wananchi wa Jimbo la Nsimbo Mkoani Rukwa kilicholenga kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zinazohusiana na masuala ya uhifadhi wa maeneo yanayosimamiwa na TAWA katika Kanda ya Magharibi, ikiwemo changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu.
Akiongea wakati wa mkutano huo Mbunge wa Jimbo hilo Anna Lupembe amesema mojawapo ya changamoto zinazowakabili Wananchi wa Jimbo lake ni pamoja na uwepo wa mamba wengi katika Mto Ugalla ambao wamekuwa wakileta madhara kwa Wananchi pamoja na masuala ya ukataji vibali kuwa mbali na makazi ya Wananchi, inayosababisha Wananchi kutumia gharama kubwa kuvifuata vibali hivyo.
Kuhusu malalamiko ya Wananchi ya kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya kukata vibali vya uvuvi na urinaji asali, Kamishna Mabula ameahidi kusogeza huduma ya ukataji vibali kutoka Wilaya ya Mlele hadi Wilaya ya Mpanda kwa ajili ya kurahisisha Wananchi kupata huduma hiyo kwa ukaribu zaidi.
Kikao hiki ni muendelezo wa ziara ya Kamishna Mabula katika kutatua changamoto mbalimbali zinazopatikana katika maeneo yanayosimamiwa na TAWA katika Kanda ya Magharibi.