Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson, ameitaka Halmashauri ya Jiji la Mbeya kuongeza jitihada ya kuwawezesha Wanafunzi wa kike katika Jiji hilo ili waweze kupata elimu katika mazingira rafiki hasa wakati wa siku zao za hedhi.
Dkt. Tulia ameyasema hayo leo tarehe 15 Agosti, 2023 wakati wa hafla ya kukabidhi taulo za kike 4000 kupitia mfuko wa Halmashauri zenye thamani ya Shilingi Milioni 10 kwa Wakuu wa Shule za Sekondari na Msingi za Serikali iliyofanyika katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari ya wasichana Loleza.
Pamoja na kuishukuru Halmashauri kwa msaada huo, amesisitiza kuwa bado idadi inayotolewa ni ndogo kulingana na uhitaji wake na ameahidi kushirikiana nao ili kuhakikisha taulo nyingi zaidi zinazopatikana kukidhi mahitaji.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya Mhe. Dormohamed Issa, amemshukuru na kumpongeza Dkt. Tulia kwa jitihada ambazo amekuwa akizifanya katika Jiji hilo ikiwemo kuwaunganisha Wananchi na Serikali yao na kuwezesha kupata mafanikio ya haraka kila kukicha.