Habari ya Asubuhi.!Karibu kwenye matangazo yetu hii leo Jumatano 16.8.2023
Wakala wa barabara nchini-TANROADS imeanza utekelezaji wa kujenga na kuunganisha mitandao ya barabara nchini kwa kiwango cha lami kwa utaratibu wa EPC+F wenye thamani ya Shilingi za kitanzania Trilioni 3.775 ambao utahusisha ujenzi wa Barabara 7 zenye jumla ya km 2,305.
TANROADS imesema barabara zinazojengwa zaidi ya kilomita 380 mkoani TANGA itaweza kukuza kukuza uchumi na pia utawanufaisha wakazi wanaoishi maeneo ya mradi kwa kuzalisha ajira zaidi ya 1000 kwa watanzania.
Mhandisi Harold Kitainda ambae ni Meneja wa miradi ya Public Private Partinerships- PPP na Engineering, Procurement, Construction and Financing (EPC +F) amesema kuwa dhumuni la mradi huo ni kuboresha mtandao wa barabara nchini na kuongeza ufanisi katika sekta ya usafiri na usafirishaji ili kuchochea uzalishaji, kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa wananchi kwa sehemu zinazopita barabara hizo na kwa Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Mhandisi Zuhura Amani ambaye ni kaimu meneja wa TANROADS mkoani TANGA amesema barabara hizo zitakapokamilika zitasaidia usafirishaji wa mizigo kutoka bandari ya Tanga kwenda mikoa mbalimbali kwa urahisi.
“Barabara hizi zinapodumu muda mrefu maana ya ni kwamba mzigo ni mdogo lakini mzigo unavyoongeza huwa zinaharibika kwa kasi sana hata muda ule ambao ulikua umekusudia barabara idumu unaweza usifike , kwahiyo itakua barabara muhimu baada ya kukamilka kwa kukuza uchumi wa mkoa wa Tanga wa nchi kwa ujumla”.
Naye Magreth Chillo ambaye ni katibu tawala wilaya ya Handeni amesema elimu inatolewa kwa wananchi umuhimu wa ujenzi wa barabara na itakapo kamilika wawekezaji watakuja na huduma za kijamii zitafikika kwa haraka na kufungua fursa mbalimbaki ikiwemo biashara ,kilimo na sekta ya madini kukua.
“Sisi kama wilaya kwanza tunamshukuru rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa maeneo yote kutuona sisi Handeni, vilevile tunaamini barabara hii inakuwa kama barabara ya kimkakati sababu inaunganisha maeneo mengi mpaka nje ya nchi, kwahiyo tunamshukuru sana na tunaamini kwamba barabara hii itakua inaenda bila kusuasua kwasaba ni hela ambazo zitatoka kwa mkupuo kwahiyo tunashukuru sana serikali ya awamu ya sita kwa mradi huu hapa Handeni”.