Zaidi ya raia milioni 1 wameondoka Sudan na kukimbilia nchi Jirani, huku wale waliobakia wanaelekea kuishiwa chakula na huenda wakafariki kutokana na kukosa huduma za afya miezi minne tangu kuzuka kwa vita, imeonya ripoti ya umoja wa Mataifa.
Kwa mujibu wa UN, mapigano kati ya jeshi na wapiganaji wa RSF yamesababisha hasara kubwa kwenye mji wa Khartoum na kusababisha machafuko mapya ya kikabila katika jimbo la Darfur na huenda vita hiyo ikatatiza usalama wa ukanda.
Muda hauko tena kwa wakulima kupanda mazao ambayo yangeweza kuwalisha pamoja na majirani zao, dawa hazipatikani na hali inazidi kuwa mbaya, hii ni sehemu ya maneno ya ripoti ya pamoja iliyotolewa na mashirika ya umoja wa Mataifa.
Aidha ripoti ya mashirika hayo imeongeza kuwa, mamilioni ya raia kwenye mji wa Khartoum na miji mingine ikiwemo Kordofan na Darfur wamekuwa wakikabiliwa na vitendo vya uporaji, kukatiwa umeme, maji na kukosa mawasiliano.
Katika hatua nyingine, afisa wa shirika la idadi ya watu duniani, Laila Baker, amesema vitendo vya matukio ya udhalilishaji wa kingoni pia vimeongezeka kwa asilimia 50 huku UNICEF yenyewe ikisema mamilioni ya wanafunzi hawaendi tena shule.