Kiongozi wa upinzani nchini Senegal ameendeleza mgomo wake wa kula tangu Julai 31, tarehe ya kufungwa kwake. Kwa siku tano zilizopita, amekataa hata kutibiwa, ili kupinga kukamatwa kwake Julai 28, baada ya kupatikana na hatia ya kutoa wito wa kuanzisha uasi. Huku hali yake ya afya ikizidi kuzorota, wanasiasa kadhaa wa upinzani wana wasiwasi kuhusu hatima yake.
Jumatano hii, Agosti 16, Ousmane Sonko hajala kwa siku 17 akiwa amefunguliwa mashtaka na kufungwa Jumatatu Julai 31, kiongozi huyo wa upinzani nchini Senegal, anayelengwa na makosa saba ikiwa ni pamoja na wito wa kuanzisa uasi, anaendelea na mgomo wake wa kula na hali yake ya afya inasababisha wasiwasi ndani ya muungano wa upinzani Yewwi Askan Wi.
Kama ukumbusho, mnamo Agosti 6, Ousmane Sonko alilazimika kulazwa hospitalini huko Dakar kwa sababu ya hali yake mbaya ya kiafya. Licha ya hayo, kiongozi wa PASTEF, chama kilichofutwa, hakubadilisha mwenendo wake. Habib Sy, mwenyekiti wa muungano wa viongozi wa Yewwi Askan Wi, anaweka wazi wasiwasi wake:
“Ousmane Sonko anaendeleza mgomo wa kula na anakataa kupewa huduma ya matibabu. Tuna wasiwasi kwa sababu mapambano anayoshiriki, anayaona yamekamilika. Na hakuna mtu anayeweza kutabiri athari ya kuzorota kwa afya yake. ”
“Tulimtumia barua ya kumtaka kusitisha mgomo wa kula. Akaamua kuendelea. Tunarudia ombi lile lile kwake, ili awe imara, ili tuendelee kuongoza pambano pamoja. ”