Mshukiwa wa mauaji ya kimbari ya Rwanda Fulgence Kayishema, ambaye amekuwa kakizuiliwa nchini Afrika Kusini, amekamatwa tena kwa amri ya kuhamishiwa Arusha, Tanzania, kujibu mashtaka ya mauaji ya kimbari.
Matukio ya hivi punde ambayo yalitokana na ombi la Mahakama Maalum ya Umoja ya Mataifa ya kushughulkikia kesi za Jinai – yanaonekana kuwashangaza wanasheria wake.
Kayishema alikamatwa akiwa katika seli za mahakama kuu mjini Cape Town mapema Jumanne.
Mahakama hiyo inamtaka ajibu mashtaka ya kudaiwa kupanga mauaji ya takriban wakimbizi 2,000 wa Kitutsi katika kanisa katoliki nchini Rwanda wakati wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.
Bw Kayishema tayari yuko kizuizini nchini Afrika Kusini baada ya kufuatiliwa katika shamba la mvinyo huko Paarl katika jimbo la Western Cape na awali alikamatwa kwa kukiuka sheria za uhamiaji za nchi hiyo.
Wachunguzi wa Afrika Kusini walisema amekuwa akiishi Afrika Kusini kwa jina la uwongo tangu kuwasili kwake mwaka 2000.
Katika nchi yake ya nyumbani, Rwanda, anashutumiwa kwa kuhusika katika mauaji ya kimbari ya 1994, kushiriki katika mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Wakati alipofikishwa mahakamani mara ya mwisho mwezi Juni, aliondoa ombi lake la dhamana na kusema kwamba angeomba hadhi ya ukimbizi nchini Afrika Kusini.
Kesi dhidi yake imeahirishwa hadi Agosti 30 ili kuruhusu mawakili wake na waendesha mashtaka wa eneo hilo kujibu amri ya kukamatwa na kuhamishiwa kwengine.