Waziri mkuu wa kiraia aliyeteuliwa na utawala wakijeshi nchini Niger, Ali Mahaman Lamine Zeine, na wajumbe wengine wawili wa baraza tawala la kijeshi walizuru Chad siku ya Jumanne kwa mazungumzo na Rais wa mpito Jenerali Mahamat Idriss Déby.
Bw Zeine, ambaye ameibuka kama uso wa kidiplomasia wa serikali ya kijeshi, alisema nchi yake sasa iko chini ya serikali ya “mpito” na akasisitiza utayari wa junta kwa mazungumzo.
Lakini, alisema utawala wa kijeshi utazungumza tu na “washirika” ambao wanaheshimu uhuru wa nchi yake.
Rais wa Chad Déby amefanya juhudi za kupatanisha kati ya serikali ya Niger na serikali iliyoondolewa madarakani ya Rais Mohamed Bazoum.
Chad pia imesema haitashiriki katika hatua zozote za kijeshi dhidi ya viongozi wa mapinduzi ya Niger.
Wakati huo huo, wakuu wa majeshi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (Ecowas) watakutana katika mji mkuu wa Ghana, Accra, siku ya Alhamisi na Ijumaa kujadili hali ya Niger.
Wakuu hao wa kijeshi wanaripotiwa kukutana ili kupanga mpango wa kuingilia kijeshi nchini Niger ili kumrejesha bwana Bazoum mamlakani.