Rais wa Nigeria, Bola Tinubu, ameomboleza vifo vya maafisa wa usalama 26, baada ya kuangushwa kwa helikopta ya kijeshi na watu wenye silaha katika jimbo la kati la Niger.
Ripoti zinasema, wote waliouawa ni wanajeshi wa Nigeria na wanane walijeruhiwa. Maofisa hao walifariki wakati wakielekea katika shughuli za uokozi katika jimbo la Niger nchini Nigeria siku ya Jumatatu.
Rais Tinubu amesema wanajeshi hao waliouawa watakumbukwa kutokana juhudi zao za kuhakikisha raia wa taifa hilo wanaishi kwa amani.
Helikopta hiyo iliyoanguka ilikuwa inaenda kuwaondoa wanajeshi wengine waliokuwa wameshambuliwa katika eneo moja ambapo jeshi limekuwa likipigana na makundi ya watu wenye silaha. Maofisa kadhaa waliripotiwa kujeruhiwa katika shambulio hilo.
Makundi ya watu wenye silaha yamekuwa yakiripotiwa kuwateka watu katikati na kaskazini mwa nchi ya Nigeria ambapo huitisha kikombozi ilikuwaachia huru.