Serikali ya wanamgambo wa Taliban nchini Afghanistan imepiga marufuku vyama vyote vya siasa nchini humo ikidai kuwa ni kinyume cha sheria za Kiislamu au Shariah.
Tangazo hilo limetolewa baada ya viongozi waliochukua madaraka ya Afghanistan kuadhimisha mwaka wa pili tangu kurejesha utawala wao mjini Kabul. Tangazo hilo limetolewa na Maulavi Abdul Hakim Sharei ambaye ni waziri wa sheria wa Taliban, wakati akizungumza na waandishi wa habari katikak mji mkuu wa nchi hiyo Kabul.
Zaidi ya vyama 70 vya siasa vilikuwa vimesajiliwa rasmi na wizara ya sheria hadi pale Taliban ilipochukua udhibiti wa taifa hilo lililokumbwa na mapigano miaka miwili iliyopita.
Tangu wakati huo, serikali ya Taliban imekuwa ikilaumiwa kwa kuminya uhuru wa kutangamana, kukusanyika na kujieleza, kama mbimu ya kunyamazisha wakosoaji, wakati wafuasi wake wakiruhusiwa kuendesha shughuli zao kama kawaida.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, serikali ya Taliban imepiga marufuku wanawake wa Afghanistan kufanya kazi katika taasisi za Umoja wa Mataifa nchini humo katika hali ambayo, kwa kipindi kinachokaribia miaka miwili tangu kundi hilo litwae madaraka, suala la elimu na ajira kwa wanawake wa Afghanistan limekuwa moja ya changamoto za mivutano iliyopo kati ya Taliban na jamii ya kimataifa.