Wakuu wa kijeshi wa Afrika Magharibi walianza mazungumzo nchini Ghana siku ya Alhamisi ili kuratibu uwezekano wa uingiliaji kati wa kutumia silaha unaolenga kurudisha nyuma mapinduzi ya Niger mwezi uliopita.
Serikali ya Niger imesema iko tayari kwa mazungumzo kutatua hali hiyo.
Lakini bado inamzuilia Rais aliyeondolewa madarakani Mohamed Bazoum na imesema itamfungulia mashitaka ya uhaini mkubwa, ambayo imeonekana kuwa ni ishara kwamba haiko tayari kutafuta njia ya amani ya kujiondoa katika mgogoro huo.
“Demokrasia ndiyo tunachosimamia na ndicho tunachohimiza,” Mkuu wa Majeshi wa Nigeria, Jenerali Christopher Gwabin Musa, aliuambia mkutano wa kambi ya ECOWAS mjini Accra.
“Lengo la mkusanyiko wetu sio tu kuguswa na matukio, lakini kuandaa kwa vitendo njia ambayo inaleta amani na kukuza utulivu.”