Idadi kubwa ya washiriki wa mkutano wa siku tatu katika Bunge la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamepiga kura kuondoa utawala wa kijeshi katika majimbo mawili ya mashariki yaliyoathiriwa pakubwa na ukosefu wa usalama uliodumu kwa muda mrefu.
Mamlaka ya kijeshi Ilichukua nafasi ya utawala wa kiraia mwezi Mei 2021 kwa lengo la kupambana na makundi yenye silaha katika majimbo ya Ituri na Kivu Kaskazini.
Lakini ripoti ya hivi punde kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Katibu Mkuu Antonio Guterres wiki iliyopita ilisema hali imekuwa mbaya zaidi katika majimbo hayo mawili, ambapo takriban watu milioni nne wameyakimbia makazi yao
“Utawala wa kijeshi haikubadilisha chochote…wananchi wamechoshwa nayo. Acha mamlaka irudishwe kwa raia,” Béatrice Nyiramugeyo, mbunge aliyeshiriki katika mkutano huo, aliiambia BBC Idhaa ya Maziwa Makuu.
Radio Okapi inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ilimnukuu Mbunge Fabrice Adenonga akisema kuwa washiriki 195 kati ya 196 wa mkutano wa mashauriano uliomalizika siku ya Jumatano walipiga kura ya kuunga mkono kuondolewa kwa hali ya kuzingirwa.
Sasa ni juu ya Rais Félix Tshisekedi “hatimaye kujibu” kuhusu suala hilo, msemaji wa serikali Patrick Muyaya aliuambia mkutano na waandishi wa habari katika mji mkuu, Kinshasa.