Mkuu wa shirika la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa Volker Turk amesema Alhamisi kwamba Korea Kaskazini imezidisha ukikukaji wa haki za binadamu, wakati watu wake wakiendelea kuvunjika moyo huku baadhi wakisemekana kukabiliwa na njaa kwenye baadhi ya maeneo.
Amesema kwamba kulingana na taarifa walizokusanya, wakazi wa taifa hilo wamekata tamaa wakati masoko yasiyo rasmi na mbinu nyingine za kukabiliana na hali waliyonayo yakivunjwa, huku hofu ya kufuatiliwa na serikali, kukamatwa, kuhojiwa na kuwekwa kizuizini ikiongezeka.
Kiongozi wa Korea Kaskazini alifunga mipaka yake katika taifa hilo la Asia kaskazini mashariki ili kudhibiti janga la Covid 19.
Lakini hata baada ya janga kumalizika, Turk amesema masharti ya serikali yameongezeka sana. Huku walinzi wa mipaka wamepewa amri ya kuwapiga risasi wageni wote wanaokaribia mipaka yake, wakati wafanyakazi wa UN wakizuiliwa pia.
Turk amekiambia kikao cha kwanza cha moja kwa moja cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa tangu 2017 kuhusu hali ya haki za binadamu nchini Korea Kaskazini, kwamba katika miaka ya nyuma watu wake wamepitia vipindi vya hali ngumu ya kiuchumi na ukandamizaji, lakini sasa hivi wanaonekana kupitia yote mawili kwa wakati mmoja.