Mamlaka nchini Kenya yamepiga marufuku makanisa matano, likiwemo lile la mchungaji anayetuhumiwa kuchochea zaidi ya wafuasi 400 kufunga hadi kufa, kulingana na waraka wa serikali uliowekwa wazi siku ya Ijumaa.
Ofisi ya Usajili wa Vyama ilisema leseni ya mtu anayejiita mchungaji Paul Nthenge Mackenzie’s Good News International Church ilikuwa imefutiliwa mbali mnamo Mei 19.
Mchungaji huyo aliyejiita kasisi alikuwa amewataka wafuasi wa vuguvugu lake kufunga hadi kifo ili “kukutana na Yesu”, kisa ambacho kiliwashangaza Wakenya baada ya kupatikana kwa maiti katika msitu wa Shakahola karibu na mji wa pwani wa Malindi.
Hadi sasa, miili 425 imepatikana katika msitu huu.
Ingawa wengi wa wahasiriwa walikufa kwa njaa, uchunguzi wa maiti pia umefichua kuwa wengine, pamoja na watoto, walinyongwa, kupigwa au kuzidiwa.
Mamlaka pia imepiga marufuku makanisa mengine manne, ikiwa ni pamoja na New Life Prayer Center na Kanisa linaloendeshwa na mwinjilisti wa televisheni anayehusishwa na Mackenzie Ezekiel Odero.
Odero anachunguzwa kwa tuhuma za mauaji, kusaidia kujiua, itikadi kali na utakatishaji fedha.
Kukamatwa kwake mwezi Aprili kulifuatia kupatikana kwa mabaki ya binadamu katika msitu wa Shakahola.
Waendesha mashtaka waliwahusisha wahubiri hao wawili, lakini Odero aliachiliwa kwa dhamana mwezi Mei, huku wiki iliyopita mahakama iliongeza muda wa kuzuiliwa kwa Mackenzie kwa siku 47 kusubiri uchunguzi zaidi.
Majaribio ya hapo awali ya serikali kudhibiti vuguvugu hizi yamekabiliwa na upinzani mkali, huku wakosoaji wakilaani ukiukaji wa dhamana ya kikatiba kuhusu kutenganisha kanisa na serikali.
Kuna makanisa 4,000 yaliyosajiliwa nchini Kenya, nchi yenye wakazi milioni 53, kulingana na takwimu za serikali.
Wengi, wakiongozwa na wachungaji wa karismatiki, wanahubiri ile inayoitwa injili ya mafanikio, wakiwataka waamini kutoa michango mikubwa kwa kanisa lao kwa ajili ya ahadi ya kuboreshwa kwa hali yao ya kifedha.