Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amewataka Watanzania kuwanyanyapaa na kuacha kuwasikiliza Viongozi wa dini au Viongozi wa siasa wanaotaka kuitumia dini kwa manufaa yao ya kisiasa kwa sababu ni kitu hatari kwa tunu ya amani na utulivu na iwapo tunu hiyo itavunjwa basi gharama yake itaonekana.
Mstaafu Kikwete ameyasema haya leo kwenye uzinduzi wa Kanisa la Waadventista Wasabato Charya Kamageta Wilayani Rorya mkoani Mara na hizi ndio nukuu zake.
“Natumia nafasi hii kukumbusha kuhusu tunu nyingine muhimu nayo ni kutokuchanganya dini na siasa tukiivunja tunu hii gharama yake tutaiona, kama kuna Viongozi wa dini wanaotaka kutuelekeza kuitumia dini kwa manufaa ya kisiasa na kama kuna Viongozi wa siasa wanataka kuitumia dini kwa manufaa yao ya kisiasa nawaombeni tuwanyanyapae, siku ikifika Uanachama wa Chama cha siasa au uumini thabiti wa dini ukawianishwa na Chama cha siasa anachokifuata ndio mwisho wa Nchi yetu”
“Mtakuwa na Vyama vya siasa vya Wakristo, Vyama vya siasa vya Waislamu, vya Walokole , Vyama vya siasa vya Watu gani, kuwafanya Watanzania kuyatazama masuala ya kisiasa, utawala na kiserikali kwa mtazamo wa dini zetu ni jambo hatari, pia Watu kutazama masuala ya dini kwa mtazamo wa siasa za Vyama vyao sio jambo lenye afya kwa Taifa letu, yote mawili yataathiri umoja na kutishia amani na utulivu tunaoufaidi hivi sasa”
“Zanzibar walifika mahali Waislamu wanamuona Sheikh ambaye ni Mfuasi wa Chama ambacho sio chake sio Sheikh sawasawa kwahiyo wakienda kuswali kama Sheikh ni Mfuasi wa CUF wanangoja amalize kusalisha halafu anaingia Sheikh wa CCM na Wafuasi wake ndio maana nilipokuwa Rais nilipambana sana kupata ule mwafaka Zanzibar”