Masoko ya magendo ya silaha nchini Sudan yamekithiri na kuibua wasiwasi mkubwa miongoni mwa raia hasa katika mji mkuu, Khartoum.
Bei ya bunduki aina ya AK-47, mojawapo ya silaha za kivita zinazotambulika zaidi, imeshuka katika kipindi cha miezi michache iliyopita kwa asilimia 50 katika soko la biashara haramu katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum.
Mfanyabiashara wa muda mrefu wa silaha amehusisha kushuka kwa kasi kwa bei ya silaha na ukweli kwamba soko la biashara haramu limejaa Kalashnikov iliyobuniwa na Russia, baada ya Sudan kutumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwezi Aprili mwaka huu.
Mapigano kati ya jeshi na Wanajeshi wa Msaada wa Haraka (RSF) hupamba moto kila siku katika mitaa ya Khartoum na miji mingine miwili, Bahri na Omdurman – ambayo inaunda mji mkuu.
Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, mfanyabiashara huyo wa silaha amesema kuwa ingawa baadhi ya wasambazaji wake ni maafisa wa jeshi waliostaafu, wengi wao wakiwa wanatoka katika jeshi la RSF.
Wakati huo huo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limetangaza kuwa, linahitaji dola milioni 400 ili kutoa msaada kwa watoto milioni 9 kati ya watoto walio katika mazingira magumu zaidi nchini Sudan.
Shirika hilo limesema kwamba kuna watoto milioni 14 wanaohitaji msaada wa haraka wa kuokoa maisha, miezi 4 baada ya kuanza mapigano ya ndani nchini Sudan, na kwamba ufadhili uliopatikana unaruhusu kutoa msaada kwa asilimia 10 tu miongoni mwao.
Serikali ya Sudan imetangaza kwamba, makadirio yanaonyesha kuwa karibu raia milioni tano wa mji mkuu wa nchi hiyo, Khartoum, na maeneo mengine wameyakimbia makazi yao.