Muungano wa vyama vinavyotawala nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, umemtuhumu aliyekuwa mwenyekiti wa tume ya uchaguzi, CENI, iliyomuingiza Rais Félix Tshisekedi, Corneille Nangaa kwa uhaini.
Haya yamejiri baada ya Corneille Nangaa, ambaye sasa ni kiongozi wa chama cha upinzani cha ADCP kuikimbia nchi yake na kwenda uhamishoni nchini Ghana, akidai kutishiwa maisha yake na utawala wa Tshisekedi.
Corneille Nangaa, ambaye tayari amejitangaza kuwa mgombea katika uchaguzi wa urais unaotarajiwa kufanyika hapa Disemba 20, alitoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka ili kuuondosha utawala wa Felix Tshisekedi, akikosoa usimamizi mbaya wa masuala ya kitaifa, uzembe na hatua zinazochukuliwa bila mipango katika sekta ya usalama.
Corneille Nangaa amesisitiza kwamba anahofia usalama wake kwani vitisho dhidi yake vilikuwa vingi baada ya kuyaonya mamlaka kuhusu hali mbaya ya nchi uhususan ile ya kiusalama. Na hivyo hayuko tayari kurejea hapa nchini hadi hali ya kisiasa itakapoimarika.
Upande mwengine Nangaa aligusia hali ambamo wapinzani kadhaa hukamatwa na kutiwa mbaroni pia wengine kuwawa kama vile mubunge Chérubin Okende, msemaji wa Ensemble pour la République, chama cha Moïse Katumbi aliyetekwa nyara na kuwawa hivi karibuni.
Corneille Nangaa ndiye aliongoza tume ya uchaguzi wakati wa uchaguzi wa rais wa Disemba 2018 na hivyo katangaza Januari 2019 matokeo na kumfaya Félix Tshisekedi kuwa raïs wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.