Takriban watoto sita wameuawa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya moto kuzuka katika kambi ya watu waliokimbia makazi yao kutokana na mafuriko.
Kambi hiyo katika mji wa Kalehe imekuwa nyumbani kwa takriban familia 420 kutoka Bushushu, kijiji kilicho kwenye Ziwa Kivu karibu na mpaka wa mashariki na Rwanda. Kijiji hicho kilikumbwa na mvua kubwa na maporomoko ya ardhi yaliyoua takriban watu 400 mwezi Mei.
Moto huo ulizuka Jumamosi mchana na kuua watoto kadhaa – “wavulana wawili wadogo na wasichana wadogo wanne, wenye umri wa mwaka mmoja hadi mitano”, amesema Thomas Bakenga, msimamizi wa eneo la Kalehe.
Amesema watu wazima wanne wamelazwa hospitalini kwa kuungua. “Moto huo ulianza kwenye kibanda katikati ya eneo ambalo mtoto alikuwa akipika wakati wazazi hawakuwepo,” amesema.
Takriban vibanda 360 vya turuba za plastiki vilivyoezekwa kwa nyasi viliharibiwa na moto huo, amebainisha. “Tulijaribu kuwaokoa, lakini haikuwa na matumaini,” Bakenga amesema. “Moto uliharibu kila kitu.”
Idadi ya wahasiriwa ilithibitishwa na mkuu wa kikundi cha kiraia cha eneo hilo, Delphin Birimbi, ambaye aliitaka serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali “kuja kusaidia wahanga hawa wa maafa”.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu ilikadiria kuwa takriban familia 3,000 zimeachwa bila makao baada ya mafuriko na maporomoko ya matope mashariki mwa DRC, eneo ambalo tayari limekumbwa na mauaji yanayotekelezwa makundi yenye silaha yanayopigana dhidi ya serikali kuu.