Wanajeshi 12 wa Niger waliuawa siku ya Jumapili katika shambulizi la kuvizia na watu wanaoshukiwa kuwa wanajihadi katika eneo la Tillabéri, kusini-magharibi mwa nchi, televisheni ya taifa, Télé Sahel, imetangaza leo Jumanne Agosti 22.
Ujumbe wa operesheni dhidi ya wanajihadi kutoka kikosi cha walinzi wa kitaifa “ulilengwa katika shambulio la kuvizia” Jumapili mwishoni jioni katika mji wa Anzourou, katika eneo lililoathiriwa vikali na ghasia za makundi haya yenye silaha, inabainisha Télé Sahel.
“Wanajeshi wetu kumi na wawili” “waliangamia,” kituo hicho kimeongeza, kikibaini kwamba “jibu” la kikosi cha walinzi wa kitaifa “lilifanya iwezekane kusababisha hasara kubwa kwa adui.”
Jimbo la Tillabéri liko katika eneo linalojulikana kama “mipaka mitatu” (ile ya Niger, Burkina Faso na Mali), kimbilio la wanajihadi wa kutoka Sahel wanaoshirikiana na Al-Qaeda na kundi la Islamic State.
Kwa miaka mingi, sehemu hii ya Niger imekuwa ikilengwa mara kwa mara na mashambulizi kutoka kwa makundi haya yenye silaha licha ya kutumwa kwa idadi kubwa ya kikosi cha kupambana na wanajihadi.
Mnamo Agosti 15, takriban wanajeshi 17 wa Niger waliuawa na 20 kujeruhiwa katika shambulio la kuvizia lililohusishwa wanajihadi katika kaunti ya Torodi, karibu na mpaka na Burkina Faso, kulingana na Wizara ya Ulinzi, kabla ya jeshi kuharibu pikipiki za washambuliaji.
“Kuzorota kwa hali ya usalama” nchini Niger ilikuwa moja ya hoja kuu zilizotajwa na wanachama wa utawala wa kijeshi kuhalalisha mapinduzi yao ya Julai 26, ambayo yalimpindua Rais Mohamed Bazoum.