Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Katavi imewafikisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi, watumishi 7 kwa tuhuma za wizi wa fedha za Halmashauri kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 1.23. Kesi hiyo ya Uhujumu Uchumi namba 5 ya mwaka 2023 imetajwa mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi wa Mahakama hiyo Gway Sumaye na mwendesha Mashtaka Gregory Mhangwa ambapo amesema watuhumiwa hao wanashitakiwa kwa makosa matatu ya kujihusisha na genge la Uhalifu, Uhujumu Uchumi na wizi.
Mhangwa ameeleza kuwa washitakiwa hao walishirikiana kutenda makosa hayo kati ya Novemba 1, 2022 hadi Agosti 11, 2023 huko katika Halmashauri ya wilaya ya Mpimbwe kwa kudanganya kuwa walikuwa wakiwalipa Wakandarasi waliofanya kazi katika Halmashauri hiyo na kuisababishia hasara Halmashauri. Washtakiwa wote hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na washitakiwa wote wamerudishwa rumande hadi Septemba 4, 2023 kesi hiyo itakapotajwa tena katika Mahakama kuu Kanda ya Sumbawanga.