Ethiopia itaanzisha uchunguzi wa pamoja na Saudi Arabia kuhusu ripoti ya Human Rights Watch inayowashutumu walinzi wa mpaka wa taifa hilo la kifalme kuua mamia ya wahamiaji kutoka Ethiopia, wizara ya mambo ya nje imesema Jumanne.
“Serikali ya Ethiopia itafanya uchunguzi haraka kuhusiana na tukio hilo sambamba na maafisa wa Saudi Arabia,” wizara hiyo ilisema kupitia mtandao wa X, uliyokuwa Twitter, siku moja baada ya kuchapishwa kwa ripoti ya HRW ambayo imezusha hasira katika pembe zote za dunia.
“Katika wakati huu tete, inashauriwa sana kujizuia kueneza uvumi hadi hapo uchunguzi utakapokamilika,” wizara ilisema, ikibainisha “uhusiano mazuri ya muda mrefu” kati ya Addis Ababa na Riyadh.
Madai hayo ambayo yameelezwa kuwa ” hayana msingi” na afisa wa serikali ya Saudi Arabia yanamulika kuongezeka kwa unyanyasaji katika njia hiyo hatari inayotokea Pembe ya Afrika kwenda Saudi Arabia, ambako maelfu ya Waethiopia wanaishi na kufanya kazi.
Shirika hilo la HRW lenye makao yake mjini New York limekuwa likiorodhesha unyanyasaji dhidi ya wahamiaji wa Ethiopia nchini Saudi Arabia na Yemen kwa kipindi cha takriban muongo mmoja sasa.