Mradi mkubwa wa maji wa kwa ajili ya kuongeza upatikanaji maji kwa Jiji la Mwanza wenye thamani ya Tsh. bilioni 69 unaojengwa eneo la Butimba kwa kutumia chanzo cha maji yanayotolewa Ziwa Victoria umefikia asilimia 94 na utaanza majaribio rasmi September 15 mwaka huu.
Kukamilika kwa awamu ya kwanza ya mradi huu kutaongeza upatikanaji wa maji Jijini Mwanza kutoka lita milioni 90 kwa siku za sasa hadi kufikia lita milioni 138 kwa siku.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema mradi huu utanufaisha Wakazi wa maeneo ya Nyegezi, Mkolani, Buhongwa, Nyamazobe, Nyahingi, Buganda, Luchelele, Lwanhima, Sahwa, Fumagila, Kishiri na Igoma kwa upande wa Jiji la Mwanza na kwa upande wa Wilaya ya Misungwi ni Usagara, Nyashishi na Fella wakati kwa upande wa Magu ni Kisesa, Bujora na Isangijo.