Mahakama nchini Kenya imebatilisha uamuzi wa kufutilia mbali leseni ya kanisa moja linaloendeshwa na mwinjilisti maarufu wa televisheni Mchungaji Ezekiel Odero.
Kituo cha Maombi ya Maisha Mapya na Kanisa katika mji wa pwani wa Kilifi huvutia maelfu ya waumini.
Jaji Jairus Ngaah alisema ilikuwa ni ahueni ya muda huku ikichunguza iwapo mamlaka ilitenda kisheria kwa kusimamisha leseni yake mwezi Mei.
Mchungaji Odero alikuwa ameendelea kuhubiri licha ya uamuzi wa Msajili wa Vyama.
Ilikuwa imeondoa leseni ya uendeshaji wa kanisa hilo lenye makao yake mjini Kilifi huku kukiwa na uchunguzi kuhusu madai ya uhusiano wa kasisi huyo na kiongozi wa madhehebu yenye utata Paul Mackenzie Nthenge.
Mchungaji Mackenzie anashikiliwa na polisi tangu Aprili kwa madai ya kuwaambia wafuasi wake wajife njaa, na kusababisha vifo vya mamia yao.
Kasisi Odero, ambaye pia alikamatwa mwezi wa Aprili lakini akaachiliwa kwa dhamana, amekana uhusiano wowote na dhehebu la njaa na kukashifu mafundisho yake.
Mawakili wake waliambia mahakama kuwa Kituo cha New Life Prayer Centre na Kanisa na biashara zake ni muhimu kwa uchumi wa Kilifi, na kuajiri watu 8,000.