Watu wasiopungua 12 wameuawa katika mapigano baina ya jamii mbili zinazozozania kipande cha ardhi huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kundi moja la kiraia liliripoti habari hiyo jana Jumatano na kueleza kuwa, mapigano hayo baina ya jamii mbili hasimu yamepelekea kuuawa raia tisa na maafisa watatu wa usalama katika mkoa wa Ituri.
Msemaji wa jeshi katika mkoa wa Ituri, Jules Ngongo Tshikudi amesema mapigano hayo ya kugombania ardhi yalizuka tangu Jumapili na kuendelea hadi Jumatatu, katika eneo lililoko baina ya vijiji vya Nyatsa na Adroval mkoani Ituri.
Tshikudi amenukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema kuwa, “Mbali na kuuawa raia (tisa), lakini pia maafisa wawili wa polisi na mwanajeshi mmoja wameuawa, huku askari wawili wakitoweka.”
Haya yanajiri siku chache baada ya waasi wa kundi linalojiita Allied Democratic Forces (ADF) kuwaua wanavijiji 55 katika mikoa ya Ituri na Kivu Kaskazini, huko huko mashariki mwa Kongo DR.
Ripoti mpya ya Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) inaonyesha kuwa, watu takriban 600,000 wamelazimika kukimbia makaazi yao kufuatia mapigano kati ya makundi ya wapiganaji wenye silaha, na jeshi la serikali mashariki mwa DRC katika muda wa miezi sita ya kwanza ya mwaka huu.