Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema Wizara yake imejipanga kuanzisha gesti za mifugo (livestock guest house)katika Ranchi za Taifa (NARCO) ili kuwapa fursa Vijana na Wafugaji wengine kuiweka mifugo yao humo kwa muda maalum ili kuiongezea thamani na kisha kuiuza kwa bei nzuri ndani na nje ya Nchi.
Waziri Ulega amesema hayo wakati wa kikao cha kuwasilisha taarifa ya hali ya sekta ya mifugo nchini kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo kilichofanyika jijini Dodoma leo Agosti 24, 2023.
Amesema Serikali ipo katika mpango wa kuweka miundombinu mizuri ikiwemo majosho na mabwawa ya kunyweshea mifugo itakayowawezesha Wafugaji kufanya shughuli zao za unenepeshaji wa mifugo na kuivuna ili kukuza kipato chao ambapo wataweka utaratibu mzuri wa kuwapata Vijana na Wafugaji wengine ambao watakuwa tayari kupeleka mifugo yao katika gesti hizo lengo likiwa kuwafanya Wafugaji waone tija ya ufugaji wa kisasa na kuondokana na ufugaji wa kuhamahama ambao umekuwa ukiwaingiza matatizoni kila uchao.
Amesema kwa kuanza wataweka miundombinu hiyo katika Ranchi ya Mkata iliyopo Mkoani Morogoro ili kuwapa nafasi Wafugaji waliopo katika Bonde la Mto Kilombero waweze kufanya ufugaji wao humo ili waondokane na ufugaji holela.