Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto siku ya Ijumaa lilionya kwamba mwaka mmoja baada ya mafuriko makubwa ya Pakistan, takriban watoto milioni 4 wanaendelea kuhitaji msaada wa kibinadamu na kupata huduma muhimu huku uhaba wa fedha ukiendelea kuwa kikwazo katika kupona.
Onyo hilo kutoka kwa UNICEF linakuja wakati mamlaka katika jimbo la Punjab mashariki mwa Pakistani zikikabiliana na wakati kuwahamisha watu kutoka maeneo yaliyoathiriwa na Mto Sutlej unaofurika.
Tangu Agosti 1, waokoaji wamewahamisha zaidi ya watu 100,000 kutoka maeneo yaliyosongwa na watu katika wilaya za Kasur na Bahawalpur.
Zaidi ya miezi sita iliyopita, makumi ya nchi na taasisi za kimataifa katika mkutano unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa huko Geneva ziliahidi zaidi ya dola bilioni 9 kusaidia Pakistan kupona na kujijenga upya kutokana na mafuriko ya majira ya joto yaliyopita ,lakini ahadi nyingi zilikuwa katika mfumo wa mikopo kwa ajili ya miradi, ambayo bado iko katika hatua za kupanga.
“Mvua za msimu huu za masika zinazidisha hali ngumu kwa jamii zilizoathiriwa na mafuriko, na kupoteza maisha ya watoto 87 kote nchini,” UNICEF ilisema katika taarifa.
Ilisema takriban watu milioni 8, karibu nusu yao ni watoto, wanaendelea kuishi bila kupata maji salama katika maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko. Ilisema zaidi ya watoto milioni 1.5 bado wanahitaji afua za lishe ya kuokoa maisha katika wilaya zilizoathiriwa na mafuriko, wakati ombi la sasa la UNICEF la dola milioni 173.5 bado linafadhiliwa kwa 57%.