Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Balozi Dkt. Pindi Chana ametoa wito kwa Wasanii kuendelea kujisajili kupitia Baraza la Sanaa ili waendeleee kunufaika na maokoto ya mikopo inayotolewa na Serikali.
Waziri amesema hayo Mkoani Njombe wakati akifungua Tamasha la pili la kitaifa la utamaduni linaloendelea kufanyika kwa siku tatu Mkoani humo ambapo Mikoa yote 31 Tanzania inashiriki katika Tamasha hilo.
“Wizara inatoa maokoto, mirabaha ipo vizuri na Rais wetu amekuja na mfuko wa kukopesha watu wa utamaduni kwa hiyo vijana mkajisajili Baraza la Sanaa mnufaike”
Dkt. Pindi Chana amewapongeza Watu wa Mkoa wa Njombe kwa ukaribisho na kuwapokea Wageni kwa kuwa huo ndio utamaduni wa Watanzania na kusema kwa sasa Wageni wanaendelea kuujua vizuri Mkoa wa Njombe, hali ya hewa na utamaduni wa vyakula vyao ikiwemo kande, numbu na ulanzi.
Kwa upande wake DC wa Njombe, Kissa Kasongwa kwa niaba ya RC wa Njombe Anthony Mtaka amesema Tamasha hilo limekuwa na umuhimu mkubwa kwenye kukuza na kulinda utamaduni huku akiwakaribisha Wageni na kushuhudia utalii wa baridi.