Kufuatia ombi la Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Fatma Nyangasa, Serikali ya Uturuki kupitia Taasisi ya Uratibu na Maendeleo ya Uturuki (TİKA) imekarabati mabweni ya Wasichana ya Shule ya Msingi Msimbu iliyopo Kisarawe na kuwapa msaada wa vitanda na magodoro.
Shule hiyo inayotoa elimu kwa Wanafunzi 1000 ipo umbali wa KM 20 kutoka Mji wa Kisarawe huku barabara ikiwa haina lami hivyo kufanya usafiri kuwa mgumu kufika Shuleni hapo na kwakuwa hakuna Shule nyingine katika maeneo ya jirani, Wanafunzi hufanya safari ya kwenda na kurudi shuleni kwa kutembea au kutumia baiskeli kila siku kwa takribani KM 8 hadi 10.
Hata hivyo, Wanafunzi 80 wa kike wanaoishi mbali zaidi (umbali wa KM 15-20) wanakaa katika mabweni ya Shule hiyo ambayo ilikuwa na upungufu wa vitanda na magodoro hali iliyosababisha Wanafunzi 80 wa kike kuishi katika mazingira duni na kuwa na vitanda 20 pekee.
Mchango huo unatajwa kuwa utaboresha siyo tu mazingira ya kuishi ya Wanafunzi bali pia utachangia katika maendeleo yao kisaikolojia na kielimu, kwa kushirikiana na Uongozi wa Shule, sherehe ya ufunguzi ilifanyika katika mabweni yaliyofanyiwa ukarabati, sherehe hizo zikihudhuriwa na Balozi wa Uturuki Dr. Mehmet GÜLLÜOĞLU, DC Fatma Nyangasa, Maafisa na Wafanyakazi wa elimu wa Wilaya, pamoja na Uongozi wa Shule na Wanafunzi.